Kocha Stewart Hall aipania Yanga FC Ngao ya Jamii
Baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame mwaka huu, Kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall, ametamba atafanya vizuri msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), huku akiahidi kuanza kwa kuifunga Yanga katika mechi yao ijayo ya Ngao ya Jamii.Azam na Yanga zitachuana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Agosti 22, mwaka huu, mechi ambayo itaashiria ufunguzi wa msimu mpya wa VPL. Katika mechi hiyo Wanajangwani watakuwa wanasaka kulipa kisasi cha kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa mwisho wa msimu uliopita wa Ligi Kuu kabla ya kung'olewa robo fainali za Kombe la Kagame mwaka huu kwa matatu 5-3.
Stewart alikaririwa katika mtandao rasmi wa Azam FC jana akieleza kuwa safu yake ya ulinzi imekuwa imara kwa sababu ndiyo aliyoanza nayo baada ya kurejeshwa kwa mara ya tatu kuwanoa mabingwa hao wa 2013/14 wa Tanzania Bara na anaamini itaendelea kumpa mafanikio zaidi kwa vile ni "msingi wa nyumba".
Hata hivyo, Stewart aliweka wazi kuwa bado hajapata soka analolitaka katika kikosi hicho cha matajiri wa Tanzania. Alisema anataka kuona timu hiyo inacheza mpira wa kutiririka na pasi za haraka.
Muingereza huyo alisema anaamini malengo hayo yatatimia wakati timu hiyo itakapokuwa mafichoni kujipanga upya na watakaporejea, watakuwa na kikosi cha maangamizi.
Imeelezwa kuwa kikosi cha Azam kitaweka kambi maalum visiwani Zanzibar kabla ya kuikabili Yanga iliyopiga kambi jijini Mbeya kusaka mbinu za kulipiza kisasi dhidi ya mabingwa hao wapya wa Afrika Mashariki na Kati.
"Timu ilikuwa imara kwenye ulinzi kwa sababu ndiko nilianza nako kutengeneza safu ya ulinzi katika timu, ninaweza kuifananisha na msingi unapoanza kujenga nyumba, unapokosea kuanzia hapo kila kitu kinaharibika," alisema Stewart na kueleza zaidi:
"Hivyo baada ya kukamilisha hili, sasa ninakwenda kujiandaa kwa mechi dhidi ya Yanga, huko nitaboresha pia safu nyingine ambazo zina upungufu. Ninaamini wakati tunarejea kila kitu kitakuwa safi."
Azam imeweka rekodi ya kutwaa Kombe la Kagame ikishinda mechi zote sita ilizocheza bila kuruhusu bao hata moja. Timu hiyo imefika fainali za michuano hiyo mara mbili ikifungwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika fainali yake ya kwanza 2012.
Ikitumia mfumo wa 3-5-2, Azam ilikuwa na safu imara ya ulinzi ambayo iliongozwa na beki matata kutoka Ivory Coast, Serge Wawa aliyeibuka Mchezaji Bora mara nne katika mechi zote sita huku akipewa zawadi ya Beki Bora na Mchezaji Bora wa michuano hiyo mwaka huu.
Tweet
Chanzo NIPASHE
0 comments:
Post a Comment