Kocha Taifa Stars amuita Manula Kikosini
Kipa kinda Aishi Manula wa Azam FC huenda akaanza kumweka benchi kipa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa sasa, Ali Mustafa 'Barthez' wa Yanga kutokana na kiwango kikubwa ambacho yosso huyo amekionyesha katika Kombe la Kagame mwaka huu akicheza mechi tano kati ya sita bila kuruhusu bao hata moja.Hatua hiyo inakuja baada ya Kocha wa muda wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa, kuliambia NIPASHE jana kuwa, michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu imemsaidia kupata wachezaji wapya atakaowajumuisha kwenye kikosi chake kitakachokwenda kambini Uturuki kujiandaa kwa mechi ngumu dhidi ya Nigeria.
Timu hiyo ya soka ya Tanzania itakuwa na kibarua kigumu mbele ya mabingwa wa zamani wa Afrika, Nigeria wakati timu hizo zitakapochuana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Septemba 5, mwaka huu kusaka tiketi ya kufuzu fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
Katika mahojiano na NIPASHE kwa simu jana, Mkwasa alisema mashindano ya Kombe la Kagame mwaka huu yaliyomalizika Jumapili huku Azam FC wakitwaa taji lao la kwanza, yamemsaidia kupata wachezaji atakaopaa nao kwenda Ulaya.
Hata hivyo, Mkwasa hakuwa tayari kuwataja kwa majina nyota hao huku akieleza kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limebariki kambi ya nje ya nchi kwa Stars na kwamba kikosi chake kitakachokwenda Uturuki kitaanikwa ndani ya siku mbili kuanzia leo.
"Bado kidogo tukamilishe orodha kamili ya wachezaji tutakaokwenda nao kambini, lakini ndani ya siku mbili tutatangaza kikosi. Kuna vijana tumewaona kwenye mashindano ya Kagame, hatutobadilisha sana kikosi chetu ila vijana hao tumewaona wameonyesha viwango vizuri, tutajaribu kuwapa nafasi," Mkwasa alisema.
“Nimepokea kwa furaha baada ya kusikia ombi letu la kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi limekubaliwa, cha msingi si kusafiri kwenda kuona mazingira, bali kuna mechi za kimataifa ambazo tayari tumeshazipata. Ninaamini zitatusaidia kujiimarisha zaidi."
Alisema tayari mawakala wao wamewataarifu kwamba Stars itacheza mechi mbili za kirafiki ikiwa kambini Uturuki. Itaanza kwa kujipima dhidi ya timu ya Taifa ya Libya Agosti 27, mwaka huu kabla ya kuikabili Kuwait au Qatar (timu hizo mbili bado hazijathibitisha).
Timu tatu za Tanzania zilishiriki michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu, Azam FC, Yanga na KMKM.
Nyota wa klabu hizo waliong'ara katika michuano hiyo mwaka huu na hawakuwa na uhakika wa namba Stars ni pamoja na winga Farid Mussa (Azam FC), mshambuliaji Mateo Antony Simon (KMKM), viungo washambuliaji Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya (wote wa Yanga).
Tweet
Chanzo NIPASHE
0 comments:
Post a Comment