Wednesday, 5 August 2015

CECAFA waipongeza AZAM FC kwa kutwaa Ubingwa #KagameCup2015

Baada la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), limeipongeza Azam FC kwa kutwaa ubingwa Kombe la Kagame mwaka huu.

Azam iliyoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2008/9, Jumapili ilitwaa taji lake la kwanza la Kagame ikiinyuka mabao 2-0 timu ngumu na ambayo ilikuwa haijafungwa katika mechi 24 mfululizo, Gor Mahia ya Kenya.

Katika taarifa yake jana, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicolaus Musonye, alisema baraza hilo linawapongeza Azam kwa kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza na kuandika historia mpya katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

"Cecafa inatumia fursa hii kuipongeza klabu ya Azam ya Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa Kagame baada ya kuifunga Gor Mahia ya Kenya katika fainali ya michuano hii Jumapili. Pia tunaipongeza Gor Mahia kwa kutoa ushindani mkali katika michuano hii mwaka huu," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo na kueleza zaidi:

"Tunatumia nafasi hii kuwapongeza mashabiki wote waliohakikisha tunafanikisha mashindano haya mwaka huu. Jumla ya timu 13 zimeshiriki Kombe la Kagame 2015 kuanzia Julai 13 hadi Agosti 2."

Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ndiye mdhamini mkuu wa mashindano hayo, alitoa zawadi ya fedha taslim USD 60,000 ambayo mabingwa Azam waliweka kibindoni USD 30,000 (Sh. milioni 62), wanafainali Gor Mahia walipata USD 20,000 (Sh. milioni 40) wakati KCCA ya Uganda ilipewa USD 10,000 (Sh. milioni 20) kwa kushika nafasi ya tatu.






Chanzo NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2014 KaribuVijana