Simba yashindwa kukwaa saini ya Mavugo
Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imesema haiko tayari kuilipa timu ya Vital'O ya Burundi kiasi cha Dola za Marekani 60,000 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji Laudit Mavugo, ambaye alikuwa akielezwa kuwa ndiye mrithi sahihi wa Mganda Emmanuel Okwi aliyejiunga na SonderjyskE ya Ligi Kuu Denmark, imefahamika.Taarifa za awali kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa Mavugo ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Burundi, alishalipwa kiasi cha Dola za Marekani 20,000 ili aweze kusaini mkataba na klabu hiyo yenye makao makuu Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini.
Chanzo cha gazeti hili kilisema Kamati ya Utendaji na Kamati ya Usajili za Simba zilizokutana mapema wiki hii, zilifikia maamuzi ya kuachana na mshambuliaji huyo kwa sababu hawaamini thamani yake inafanana na kiasi hicho cha fedha kinachotakiwa na Vital'O kuipata saini ya Mavugo.
"Hatuwezi kumsajili kwa dau la Dola (za Marekani) 80,000, hana thamani hiyo, ndivyo tulivyoamua, na maamuzi yetu yamezingatia Simba haishiriki mashindano makubwa mwakani," kilieleza chanzo chetu cha uhakika ndani ya klabu hiyo.
Chanzo hicho kilisema wanaishangaa Vital'O kwa kutokuwa wa kweli katika maamuzi yao ya kumuuza mshambuliaji huyo ambaye hivi karibuni aliwafungia mabao yote katika ushindi wa 2-1 na kubeba Kombe la FA.
"Tulianza nao mazungumzo vizuri, lakini siku zilivyokuwa zinakwenda, walikuwa wakipandisha dau, mchezaji mwenyewe tayari alikuwa ameridhia kujiunga Simba na makubaliano binafsi yalikuwa yamekamilika na kilichokuwa kimebakia ni kumalizana na timu hiyo ambayo Simba si mara ya kwanza kusajili mchezaji kutoka kwao," aliongeza.
Rais wa Simba, Evans Aveva, jana hakupatikana kuelezea maamuzi hayo yaliyofikiwa na Kamati ya Utendaji kwa kushirikiana na ile ya Usajili inayoongozwa na Zacharia Hanspoppe.
Julai 23, mwaka huu, Aveva aliliambia gazeti hili, "Mavugo atatua nchini siku yoyote wiki hii," jambo ambalo limekwama hadi kufikia jana muda mchache kabla hatujaenda mitamboni.
Mavugo amewahi kukaririwa na vyombo mbalimbali vya habari kutoka Bujumbura, Burundi akisema yeye hana tatizo la kuja Tanzania, ila Simba inatakiwa imalizane na klabu yake kwanza.
Wakati huo huo, habari kutoka Zanzibar zinaeleza kuwa benchi la ufundi la timu hiyo limemkataa aliyekuwa kipa wa timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20, timu ya Chelsea ya Uingereza, Vincent Depaul Angban, kuendelea kufanya majaribio.
Kipa huyo ambaye alianzia kufanya majaribio ya kutaka kusajiliwa kwenye timu ya Azam, amerejea jijini jana baada ya Wekundu wa Msimbazi kutoridhishwa na kiwango chake.
Habari zilizopatikana jijini zinasema kuwa bado Kamati ya Usajili ya Simba inaendelea kusaka kipa mpya na mshambuliaji mmoja ambaye ataziba pengo lililoachwa na Okwi.
"Yule kipa wa Ivory Coast amekataliwa, ila kamati baada ya kuiangalia timu ikifanya mazoezi na mechi tuliyocheza na Kombaini ya Zanzibar, tunahitaji wachezaji wawili muhimu, kipa na mshambuliaji aliyeiva," alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Simba.
Aliongeza kuwa baada ya kupata wachezaji hao wawili, kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kitakuwa kimekamilika tayari kusubiri msimu mpya wa Ligi ya Bara Kuanza hapo Septemba 12, mwaka huu.
Awali Simba ilikuwa na mpango wa kumsajili kipa wa Gor Mahia, Boniface Oluoch, lakini wameamua kuachana naye kutokana na klabu yake kudata la Dola za Marekani 100,000, hiyo ikitokana na ofa nyingine kutoka Afrika Kusini ambayo wameipokea.
Wekundu wa Msimbazi pia wameamua kuachana na harakati za kutaka kumsajili mshambuliaji wa Gor Mahia, Michael Olunga, kufuatia mchezaji huyo kutaka dau la Dola za Marekani 200,000 na klabu Dola za Marekani 50,000.
Rais wa Simba Evans Aveva
Chanzo NIPASHE
0 comments:
Post a Comment