Wednesday, 5 August 2015

Ben Pol Atisha Coke Studio Africa Huko Nchini Kenya

Msimu wa tatu Coke Studio Afrika umeanza kwa wasanii Ben Paul kutoka Tanzania, Wangechi (Kenya) na Silver Stone wa Ghana kutumbuiza katika jukwaa la Coke Studio na kuamsha nderemo na vifijo kwa mashabiki ambao walihudhuria tamasha hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki hii nchini Kenya.

Wimbo ulioonekana kukonga nyoyo za mashabiki katika tamasha hilo ni ‘Sophia’ wa Ben Pol aliouimba kwa kushirikiana na Wangechi.

Msimu huu wa Coke Studio umeambatana na kampeni mpya yenye jina la ‘Sababu Bilioni za Kujiamini’, na hivyo kujumuisha vijana mbalimbali ambao wanaamini katika kufikia malengo yao bila ya kujali changamoto zinazowakabili.

Katika tamasha hilo kulikuwa na vijana watano kutoka Tanzania wenye vipaji mbalimbali ambao walipata fursa ya kujifunza kupitia mambo mbalimbali baada ya kueleza namna wanavyojiamini katika kutimiza ndoto zao.

Vijana hao ni Minaeli Benedict, Stanley Meshack Mafundo, Hassan Singizi, Jackson, Shabani Swaibu (wote kutoka Dar es Salaam) na Jackson Kassian (Morogoro).

Baada ya kumalizika kwa tamasha hilo, vijana hao walipata fursa ya kuzungumza na wasanii hao ambao pia ni vijana kabisa, na kuelezwa mbinu ambazo zitawawezesha kupambana na hatimaye kufikia ndoto zao.

Katika kuhakikisha vijana hao hawakati tamaa kufikia malengo yao, Ben Pol aliwaambia kwamba kufikia mafanikio aliyonayo sasa, amepitia changamoto nyingi sana ikiwamo kunyimwa nafasi ya kurekodi nyimbo zake na waandaaji mbalimbali wakiamini kuwa hakuwa na uwezo wa kuimba, lakini licha ya kufanyiwa hivyo aliendelea kupambana hadi kufanikiwa kufika alipo sasa.

“Ninachotaka kuwaambia ni kwamba, mfano, kwa wale wenye vipaji vya kuimba, kitu kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuwa na nyimbo nyingi ambazo, hata ukirekodi mmoja usipofanya vizuri, unatoa mwingine ili kuhakikisha unaendelea kusikia masikioni kwa watu,” alisema.

“Kitu kingine ni kwamba unaposimama mbele ya watu, waone ni wa kawaida tu na wala usiwaogope, bila ya kujali nyadhifa zao isipokuwa kikubwa ni kutowaonesha dharau,” alisisitiza.

Wangechi kwa upande wake alisema: “Vijana wa jinsia zote ni muhimu kujiamini na kuondokana na dhana kwamba jinsia fulani ndiyo wanaweza kitu fulani.

"Kwa mfano mimi naweza kufanya ‘hiphop’ na R&B, sasa wasichana wengi hata kama wanaweza, huogopa kufanya hiphop wakiamini kwamba ni muziki wa kiume, kumbe yeyote anaweza kuimba.”

Lengo kuu la Coke Studio Afrika ni kuwakutanisha kwa pamoja wasanii mbalimbali wa Afrika na kuimba nyimbo ambazo zina vionjo tofauti hivyo kuongeza msisimko. Lakini vilevile kutoa fursa kwa wasanii wachanga kushirikiana na wakubwa ili kuwapa changamoto ya kuongeza ujuzi katika kazi zao na kuzidi kukuza vipaji vyao.

Katika msimu huu wa Coke Studio Afrika, ni wasanii kutoka mataifa matano tu ndiyo wamechaguliwa kutumbuiza. Mataifa hayo ni Nigeria, Msumbiji, Kenya, Uganda na Tanzania.






Chanzo NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2014 KaribuVijana