Wednesday, 29 July 2015

Yanga je wataweza kuvunja rekodi yao dhidi ya Azam FC leo?


Wakati Yanga na Azam FC zitakumbushia fainali za 2012 ya Kombe la Kagame zitapokutana leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, Hans van der Pluijm, amesema atawathibitishia kuwa Wanalambalamba walipangwa katika kundi dhaifu la michuano hiyo mwaka huu.

Mechi hiyo ya robo fainali ya mwisho ya michuano hiyo mwaka huu, itachezwa kuanzia saa 9:45 alasiri ikishuhudiwa Yanga ikikosa huduma ya mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Liberia, Kpah Sherman ambaye juzi alikwenda Afrika Kusini kufanya majaribio.

Kitakwimu katika michuano hiyo ya Kombe la Kagame mwaka huu, kwa timu hizo mbili, inaonyesha safu ya ulinzi ya Azam ni imara zaidi kutokana na kutoruhusu bao hata moja wakati pia washambuliaji wake wakifumania nyavu mara nane.

Yanga yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili huku ikifunga mabao saba, hivyo itakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha inavunja rekodi ya Azam ya kutoruhusu bao kwenye michuano hiyo.

Katika mahojiano na NIPASHE kwenye Uwanja wa Taifa jana wakati wa mapumziko ya mechi ya robo fainali ya kwanza ya Kombe la Kagame kati ya APR na Al Khartoum, Pluijm alitamba kuwa kikosi chake kiko vizuri na anasubiri muda ufike kuonyesha udhaifu wa Azam FC.

"Azam wamefanya vema katika hatua ya awali kutokana na aina ya timu walizopangwa nazo. Sisi (Yanga) tulipangwa Kundi A ambalo lilikuwa na timu imara kuliko walizocheza nazo Azam. Kesho (leo) mtaona tutakachokifanya dhidi ya Azam.

"Najua mechi haitakuwa rahisi, na hii si kwa sababu tunacheza na Azam, hata ingekuwa timu nyingine, hatua ya mtoano ni ngumu na ina changamoyo zaidi, kila upande unahitaji kusonga mbele kwenye mashindano", alisema Pluijm.

Raia huyo wa Uholanzi alisema wachezaji wake wote wako vizuri kiafya na hana hofu ya kutolipa kisasi cha kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC katika mechi yao ya mwisho.

Wanajangwani walitwaa ubingwa wa tano wa michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati walipokifunga kikosi cha kocha Muingereza Stewart Hall mabao 2-0. Shukrani kwa mabao ya Hamis Kiiza dakika ya 44 na Said Bahanunzi aliyefunga la pili dakika za majeruhi.

Kuelekea mechi ya leo, Hall amesema anahitaji kufanya vizuri zaidi ya ilivyokuwa 2012 na anaamini mfumo wake wa 3-5-2 hautamwangusha.

Tangu arejeshwe kwa mara pili kuinoa Azam, Hall amekuwa akijikita katika kufundisha soka la mfumo huo akitumia mabeki watano, viungo watatu na washambuliaji wawili.

Mfumo huo umempa ushindi katika mechi nne za kirafiki na tatu za Kundi C la Kombe la Kagame alizoshinda 1-0 dhidi ya KCCA FC ya Uganda, 2-0 dhidi ya Malakia FC ya Sudan Kusini na 5-0 dhidi ya Adama City ya Ethiopia.

"Siiogopi timu yoyote, mfumo wetu mpya haujatuangusha katika mechi zote saba tulizocheza (nne za kirafiki).

"Timu yangu iko tayari na inajiamini itafanya vizuri, tumejipanga na nina wachezaji bora wenye uchu wa mafanikio," alisema Hall. Katika mahojiano na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana na kueleza zaidi kuwa kikosi chake hakina mchezaji aliye majeruhi.

TAKWIMU ZA KAGAME 2015
Yanga iliyokuwa Kundi A, ilimaliza nafasi ya pili katika kundi hilo ikipoteza mechi ya kwanza 2-1 dhidi ya Gor Mahia) kabla ya kushinda tatu za mwisho 3-0 dhidi ya Telecom FC ya Djibouti, 2-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar na 1-0 dhidi ya Al Khartoum ya Sudan.

Katika mechi tatu za hatua ya makundi, Azam mbali na kutoruhusu kufungwa bao hata moja, ilionyesha kucheza kwa nidhamu kubwa ikipata kadi tatu za njano (Didier Kavumbagu, Erasto Nyoni na Himid Mao).

Mshambuliaji Kipre Tchetche mwenye magoli matatu, alianzia benchi katika mechi zote mbili za mwanzo za Kundi C kabla ya kuanza katika kikosi cha Hall kilichoshinda 5-0 dhidi ya Adama City kwenye mechi ya mwisho.

Kuna uwezekano mkubwa raia huyo wa Ivory Coast kuanza katika safu ya ushambuliaji ya Azam FC leo pamoja na straika wa usajili mpya, Ame Ally Amour kutokana na kurejea katika makali yake huku nahodha John Bocco 'Adebayor' aliyefunga mabao mawili akitarajia kuanzia benchi.

Yanga iliianza kwa kuonyesha utovu wa nidhamu katika mechi ya kwanza baada ya mshambuliaji wake Mzimbabwe Donald Ngoma kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu katika michuano hiyo mwaka huu huku beki Mwingi Haji Mngwali na Zutah wakionyeshwa kadi za njano.

REKODI ZA AZAM vs YANGA
Katika mechi 14 za misimu saba iliyopita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) tangu Azam ipande Ligi Kuu, timu hizo zilitoka sare mara nne huku kila moja ikishinda mechi tano.

Katika mechi hizo, Yanga ndiyo iliyofunga mabao mengi zaidi ikitikisa nyavu za Azam mara 20 wakati Wanalambalamba walifunga mabao 19.

Aidha, Yanga iliibuka na ushindi wa 1-0 na 3-0 Azam katika mechi zote mbili zilizopita za Ngao ya Jamii kuashiria ufunguzi wa misimu miwili iliyopita ya VPL. Mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara.


Chanzo NIPASHE



















0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2014 KaribuVijana