Azam, APR zatinga robo fainali.
Azam imejihakikishia kucheza hatua ya robo fainali baada ya kuichapa mabao 2-0 Malakia ya Sudan Kusini katika mechi ya Kundi C ya michuano ya Kombe la Kagame iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.Katika mchezo huo ambao Pascal Wawa aliibuka Mchezaji Bora wa Mechi na kupewa zawadi ya king'amuzi chenye kiwango cha HD na DStv, ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha pointi sita kutokana na kushinda mechi yake ya kwanza dhidi ya KCCA ya Uganda.
Azam ambayo itashuka tena dimbani Jumamosi kumaliza mechi za hatua ya makundi kwa kuikaribisha Adama City kutoka Ethiopia, sasa inaungana na APR ya Rwanda iliyofuzu jana hatua ya robo fainali.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, baada ya mechi alisema walicheza kwa weledi kulinganisha na jinsi walivyocheza dhidi ya KCCA Jumapili.
Alisema anaendelea na mfumo wake wa sasa wa kutumia mabeki watano, wawili kati yao wakicheza katika nafasi za mawinga.
Tangu arejeshwe kwa mara ya pili kuinoa Azam FC, Muingereza huyo amekuwa akitumia mfumo wa 3-5-2.
Kuhusu kumtumia Tchetche kwa dakika 45 pekee za kipindi cha pili katika mechi mbili mfululizo, Hall alisema: "Ni suala la utimamu wa mwili. Tchetche hajarejea katika kiwango chake ndiyo maana ninamtumia kwa muda mfupi."
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Malakia FC, Ramzi Sebit, alisema: "Azam wametupa changamoto kubwa, wamecheza vizuri na wana wachezaji wengi wazuri na waliozoeana. Sasa tunalazimika kushinda mechi ya mwisho dhidi ya KCC ili tufuzu robo fainali."
MAMBO YALIKUWA HIVI...
Mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' aliifungia Azam FC bao dakika ya 26 akifumua shuti kali la mguu wa kulia baada ya kutengenezewa na kiungo Salum Abubakar 'Sure Boy' mpira wa faulo iliyotolewa na refa Davies Omweno kutoka Kenya kutokana na nahodha huyo wa Wanalambalamba kukwatuliwa na beki wa kati, Lubari Zeriba nje kidogo mwa boksi la Kaskazini mwa Uwanja wa Taifa.
Lilikuwa bao la pili kwa Bocco katika mashindano hayo baada ya kufunga pia bao pekee lililowapa ushindi wa 1-0 dhidi ya APR FC ya Rwanda kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili.
Malakia ndiyo waliopata nafasi nyingi za kulifikia lango la wapinzani wao, lakini mashuti yao matano yaliyopigwa na Soh koodjou Mfomo dakika za 7 na 12, Saddam Opera dakika za 10 na 33 pamoja na Mahmoud Al Taher dakika ya 39 hayakulenga lango la Azam FC lililokuwa chini ya ulinzi wa kipa kinda Aishi Manula.
Mbali na shuti la Bocco lililowapa bao Azam FC walipiga shuti moja tu langoni mwa Malakia kipindi cha kwanza. Shuti hilo lilipigwa na beki wao wa kati Serge Wawa na lilidakwa na kipa Kennedy Santolino katika robo saa ya mchezo.
Hadi kufikia mapumziko, Azam inayoshiriki kwa mara ya pili mashindano haya ya Kombe la Kagame, ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lakini timu zote zinalionyesha kushambuliana kwa zamu dakika hizo 45 za mwanzo.
Malakia ambayo inavaa jezi nyekundu, washambuliaji wake hawakuwa makini katika umaliziaji wakati kwenye safu ya ulinzi, beki wa kati wa Malakia, Yengo Son, alijitahidi kuokoa mipira ya hatari iliyokuwa inaelekea langoni mwao.
Dakika ya 10, Bocco alishindwa kumalizia krosi safi iliyopigwa na Gadiel Michael ambaye aliwatoka mabeki wa Malakia.
Kipindi cha pili kilipoanza Azam ilifanya mabadiliko mawili baada ya kumtoa Ammy Ali na nafasi yake kuchukuliwa na Kipre Tchetche huku Farid Mussa akiingia badala ya Gadiel Michael.
Dakika ya 51 mshambuliaji mtokekea benchi Kipre Tchetche aliifungia Azam FC bao la pili akimalizia kwa shuti mtoto la mguu wa kulia krosi iliyopenyezwa ndani ya sita na beki wa pembeni Shomari Kapombe kutoka wingi ya kulia.
Kipa wa Malakia aliwanyima Azam mabao zaidi baada ya dakika ya 60 kupangua shuti la Kipre aliyeunganishiwa krosi ya Sureboy huku dakika tano baadaye akipangu kwa mkono mmoja mpira wa kichwa uliopigwa na Bocco.
Azam pia ilimtoa Salum Abubakar katika dakika ya 64 na kumuingiza Mudathir Yahya, wakati dakika ya 72 Malakia wakifanya mabadiliko kwa kumtoa Mahmoud Taher na nafasi yake kuchukuliwa na Gabriel John. Mabadiliko mengine ya Malakia inayotoka Sudan Kusini yalikuwa katika dakika 84, Gasim Lado aliingia kuchukua nafasi ya Soh Mfomo.
Katika dakika ya 65, Kapombe alikuwa na nafasi ya kufunga bao la tatu, lakini shuti lake la mguu wa kulia likatoka nje kidogo mwa boksi baada ya kugonga besela. Hata hivyoi mpira ulirudi ndani ya boksi kisha kichwa cha Bocco hakikuwa makini kulenga langoni.
Azam FC: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Jean Mugiraneza, Frank Domayo, Salum Abubakar, Ame Ally, Kheri Salum na John Bocco.
Malakia: Kennedy Santolino, David Dada, Makir Albino, Lubari Zeriba, Wisely Onguso, Saddam Opera, Samuel Sskamatte, Mahmoud Al Taher, Ahmed Sani, Soh koodjou Mfomo na Yenga Son Ngum.
AZAM YAMNASA WANGA
Katika hatua nyingine, Azam jana imemsainisha Mkenya Allan Wanga, mkataba wa mwaka mmoja na mchezaji huyo kurejea kwao huku ikielezwa kwamba atarudi jijini Dar es Salaam Jumapili kuungana na klabu yake mpya.
APR NAYO ROBO FAINALI
Katika mechi nyingine ya Kundi B, iliyopigwa Uwanja wa Karume jana, APR ya Rwanda ilikata tiketi ya kucheza robo fainali baada ya kuichapa Heegan FC ya Somali kwa mabao 2-0. Katika mechi ya kwanza dhidi ya Al Shandy ya Sudan, APR ilishinda bao 1-0.
Chanzo NIPASHE
0 comments:
Post a Comment